KAMANDA wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM (UVCCM), Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu, Rameck Airo, ametangaza kugombea Ubunge katika Jimbo la Rorya, linaloshikiliwa Profesa Philemon Sarungi (CCM).
Airo ambaye ni miongoni mwa watu walio mstari wa mbele katika kutoa misaada mbalimbali ya kijamii ikiwemo kusomesha watoto wasio na uwezo, ametangaza nia yake hiyo jana jijini Mwanza, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema, ameamua kujitosa katika kinyang'anyiro hicho kupitia CCM kutokana na msukumo wa jamii, pamoja na kulinusuru jimbo hilo lisiende na kambi ya upinzani kwani Profesa Sarungi amelitumikia kwa muda mrefu na anapaswa apumzike.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nataka nigombee ubunge jimbo la Rorya, yapo mambo mengi yaliyosababisha nifikie uamuzi huu, ikiwa ni pamoja na kulinusuru jimbo lisiende na upinzani.
Alibainisha kuwa iwapo atafanikiwa kuwa mbunge wa Rorya ataweka utaratibu maalumu kwa watoto yatima na wanaotoka kwenye familia zisizokuwa na uwezo wilayani humo kusomeshwa bure, kwa kulipiwa karo za shule, pamoja na michango ya madawati.
Airo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Horyo, alisema watoto wengi yatima wakiwemo wanaotoka katika familia duni katika wilaya hiyo wanashindwa kuendelea na masomo yao ya sekondari, licha ya kufauli elimu ya msingi, hivyo atatumia nafasi yake ya ubunge kuhakikisha sekta ya elimu na nyinginezo zinaboreshwa zaidi.
“Kero kubwa sana katika wilaya yangu ya Rorya ni watoto kutokwenda shuleni kwa sababu ya wazazi kuwa na uwezo mdogo, mimi nasema watoto yatima na wenye wazazi wasiokuwa na uwezo watapata msaada wa kusomeshwa,” alisema.
Kuhusu maendeleo ya jimbo, kamanda huyo wa UVCCM alimpongeza Profesa Sarungi kwa juhudi alizozifanya katika kuleta maendeleo ya jimbo hilo, na kwamba ataendeleza yale yote mazuri yaliyofanywa na mbunge anayemaliza muda wake.
Hata hivyo, Airo alisema shabaha yake nyingine ni kuhakikisha anafuatilia kikamilifu bajeti ya miradi yote ya maendeleo inayopitishwa serikalini kwa ajili ya wilaya na jimbo lake kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kujenga mtandao mpana wa kuvutia wawekezaji wilayani humo kutoka ndani na nje ya nchi, kuboresha sekta ya afya na maji.
Airo alisema atatumia uwezo wake wa kibiashara kuwashawishi wafanyabiashara wenzake wa ndani na nje ya nchi kusaidia maendeleo ya wananchi wa Rorya, mkoa na taifa kwa ujumla.
.